Friday, July 20, 2012

RAISI WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI DR ALI MOHAMED SHEIN AWASISITIZA WAISLAM KUWA WATUMIAJI WAZURI WA MISKITI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, amewasisitiza Waumini wa dini ya Kislamu kutoitumia misikiti kuwa vivutio vya kusababisha uhasama, malumbano au kuwafarakanisha waumini na watu wengine.
 
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa msikiti wa Rahmatullah uliopo Mwanyanya, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ambapo viomngozi mbali mbali wa dini, vyama na serikali walihudhuria akiwemo Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
 
Katika hotuba yake Dk. Shein alieleza kuwa  misikiti iwe kwa ajili ya ibada pamoja na kuendeleza elemu miongoni mwa waislamu.
Alisema kuwa ni dhahiri kuwa mwenye elimu ana fursa zaidi na uwezo wa kufanya ibada kwa usahihi ambapo kubwa zaidi huongeza na kuimarisha ucha Mungu wake  hivyo aliwataka Waislamu kuitumia misikiti kujiongezea maarifa ya dini na sio kinyume yake.
 
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa tarekh ya Kislamu inaelezea kuwa misikiti imetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Uislamu ambapo misikiti wakati wa Mtume Muhammad S.A.W ilikuwa sio pahala pa kusali tu bali ilitumika kwa shughuli kadhaa.
 
“Kwa wakati ule kwa mfano ilikuwa ni Ikulu, mahakama, kituo cha elimu, ukumbi wa majadiliano na kadhalika… kwa zama hizi, misikiti yetu mingi hutumika zaidi kwa sala na baadhi ya darsa hasa katika mwezi wa Ramadhan na harusi au halili”,alisema Alhaj Dk. Shein.
 
Alisema kuwa huu ni wakati wa kuangalia fursa nyengine ambazo zinaweza kuitumia misikiti kwa manufaa mengine yanayoendana na mafundisho ya dini.
 
Aidha, Alhaj  Dk. Shein alisema kuwa mafundisho ya dini ya Kiislamu yanawabashiria malipo mema mbele ya Allah watu wanaoamua kutabaruku katika masuala mbali mbali ya kujenga na kuusimamisha Uislamu yakiwemo ujenzi wa misikiti, madrasa, kuchimba visima vya maji na kuwasaidia watu wenye shida.
 
Dk. Shein aliwaombea kwa Mwenyezi Mungu kuipa kila la khreri familia ya Bwana Khamis Hafidh kwa hekima na busara zao za kutoa eneo la Kiwanja cha msikiti huo pamoja  kumuombea kheri mfadhili mkuu wa sikiti huo Sheikh Ahmed Said Marekh.
 
Alhaj Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuwatanabaisha wananchi wanaoishi eneo hilo la Mwanyanya kuwa waelewe kuwa wana amana mbele ya Waislamu na wananchi wengine wanaotumia maji yanayotoka kwenye kianzio cha eneo hilo.
 
Alieleza kuwa amana waliyonayo ni kuhakikisha kuwa wanakilinda kiazio hicho dhidi ya vitendo vyote vya uharibifu wa mazingira.
 
Alisisitiza kuwa kila mtu ahisi ana wajibu wa kukihami chanzo hiki kwa kutojenga karibu nacho, kutokata miti na kuepusha hujuma yo yote itakayochangia kuzidi kupungua kima cha maji kinachopatikana katika kizio hicho.
 
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Uislamu unafundisha kuwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa ni mwezi wa mavuno kwani amali za waja huwa na malipo makubwa zaidi hivyo  wauminu wana wajibu wa kuzidisha amali njema ili waweze kunufaika na Baraka za mwezi hu.
 
Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wa Mwanyanya kuunga mkono mipango ya maendeleo ya serikali kwa kushirikiana na viongozi kwa kuendelea kudumisha amani na mshikamano wao hasa wakati huu wanapoelekea kwenye uchaguzi wa Mwakilishi wa Jimbo lao utakaofanyika mwezi wa Septemba mwaka huu pamoja na ushiriki wa sensa.
 
Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Mwanyanya kuwa Serikali itajitahidi kushirikiana na viongozi wao katika kukamilisha ujenzi wa skuli na hospitali zilizoanzishwa na wananchi katika Wadi ya Mwanyanya ili kumaliza kwake kuweze kusaidia kuondoa usumbufu wanaoupata wananchi wa eneo hilo wa kuzifuata huduma hizo maeneo ya mbali.
 
Nae mwakilishi wa mfadhili wa msikiti huo Mhe. Mohammed Raza alitoa wito kwa Waislamu kujitolea katika kuimarisha Uislamu na kueleza kuwa kwa niaba ya wafanyabiashara wanaipongeza serikali kwa kuondosha kodi kwa vyakula katika kipindi cha mwezi wa Ramadhan.
 
Aidha, Mhe Raza alisisitiza kuwa hakuna haja ya kuwepo malumbano ya Waislamu katika kugombania madhehebu huku akiwataka wafadhili wa misikiti mara wanapomaliza ujenzi wawakabidhi wananchi wenyewe husika misikiti ili wawewe kupanga mipango yao ikiwemo uongozi.
 
Nao waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wa Mwanyanya walitoa shukurani zao kwa mfadhili wa msikiti wao huo mpya wenye kusaliwa  na watu zaidi 250 na kuahidi kuudumisha na kuuendeleleza kwa lengo la kuuimarisha Uislamu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment